Taarifa
hii ikufikie mtu wangu wa nguvu kutoka Afrika Mashariki. Mamlaka nchini
Kenya imetangaza zawadi ya dola elfu 20 za kimarekani kwa taarifa zozote
zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa wa ugaidi anayetafutwa kwa
tuhuma za kupanga shambulizi katika mji wa pwani wa Lamu.
Wizara ya
mambo ya ndani ya Kenya imesema, mtuhumiwa huyo, Ramadhani Kioko,
anadaiwa kuhusika na shambulizi la kigaidi lililotokea Lamu ambapo
askari watano wa jeshi Kenya walijeruhiwa baada ya gari lao kukanyaga
bomu lililotegwa kando ya barabara Julai 26 mwaka huu. Wizara hiyo pia
imesambaza picha za mtuhumiwa huyo ambaye wanaamini kuwa alitega bomu
hilo katika eneo la Ishakani, mashariki mwa mji wa Lamu.
Hatua hiyo
imekuja baada ya wizara hiyo kutangaza zawadi ya dola elfu 20 za
kimarekani kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa
kwa mtuhumiwa mwingine wa ugaidi Abdullahi Abdi Sheikh, ambaye anadaiwa
kupanga mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi ikiwemo shambulizi
lililoshindwa dhidi ya kambi ya jeshi ya Baure kwenye kaunti ya Lamu.
No comments:
Write comments